Kampeni ya usalama barabarani ya ‘Gerayo Amahoro’ "Yaani fika kwa Amani" imendelezwa hii leo Jumatatu, Julai 14, ambapo Polisi ya Rwanda imewakumbusha watumiaji wa barabara, hususani waenda kwa miguu, kuchukua tahadhari ili kuzuia na kupunguza idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na ajali za barabarani.
Msemaji wa Kitengo cha Polisi cha Usalama Barabarani, Superintendent wa Polisi (SP) Emmanuel Kayigi, alieleza madhara mbalimbali yanayosababishwa na ajali, huku akiwaasa waenda kwa miguu kutambua kuwa wao ni washirika muhimu katika kuzuia ajali.
Alisisitiza kuwa wanapaswa kuwa na mchango dhati katika kuhakikisha usalama barabarani.

Alisema: “Ajali huleta athari nyingi kwa mhusika, familia yake na taifa kwa ujumla. Wale wasiofariki kutokana na ajali huachwa na ulemavu, huwafanya wenza wao kuwa wajane na watoto kuwa mayatima. Ajali pia husababisha matatizo mengine kama kupoteza matumaini ya maisha. Ni muhimu kila mmoja kuwa mwangalifu barabarani na kujiepusha na kosa lolote linaloweza kusababisha ajali.”

Kampeni hii ya uhamasishaji ilifanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji la Kigali, ikilenga zaidi watembea kwa miguu. Iliambatana na ujumbe wa kuwakumbusha umuhimu wa kuwa waangalifu na kuepuka uzembe pamoja na makosa yanayoweza kusababisha ajali.

Bagabo John
