Mafunzo ya maafisa Rwanda Correction Service (RCS) wa ngazi ya pili (Basic Officer Training Course Intake 02) yalianza tarehe 06 Januari 2025 yakiwa na wanafunzi 152, wakiwemo wanawake 25.
Hata hivyo, kutokana na ugumu wa mafunzo hayo, wanafunzi sita hawakuweza kuyamaliza kwa sababu mbalimbali zikiwemo matatizo ya kiafya, kushindwa masomo pamoja na kutokidhi maadili na mienendo inayotakiwa kwa watumishi wa RCS.
Kati ya wanafunzi waliohitimu mafunzo hayo, 84 tayari walikuwa ni watumishi wa kawaida ndani ya RCS , huku wengine 62 wakitoka katika maisha ya kiraia. Miongoni mwa wahitimu hao, wanawake walikuwa 21.

Waziri wa Usalama wa Ndani , Dkt Vincent Biruta, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alianza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Rwanda kwa kumuamini na kumpa mamlaka ya kumwakilisha katika sherehe hiyo, pamoja na kuwashukuru wote waliohudhuria.

Waziri wa Usalama wa Ndani , Dkt Vincent Biruta
Pia alilipongeza shule ya mafunzo ya Jeshi la Magereza nchini Rwanda, RCS Training School, kwa juhudi na kujituma kwake katika kuimarisha ubora wa taasisi hiyo. Aidha, aliwapongeza maofisa waliohitimu mafunzo hayo kwa nidhamu na mwenendo mwema waliouonyesha wakati wote wa mafunzo, jambo lililowezesha kutunukiwa cheo cha Assistant Inspector.

Aliwakumbusha kuwa taifa lina matarajio makubwa kwao, akiwataka kutolivunja moyo taifa lililowaamini na kuwapa dhamana hiyo.
Bagabo John
