Timu ya APR FC kutoka Rwanda imepangwa katika Kundi B kwenye mashindano ya CECAFA Kagame Cup ya mwaka 2025. upangaji wa makundi ilifanyika hivi karibuni, ambapo timu mbalimbali kutoka kanda ya Afrika Mashariki na Kati zimegawanywa katika makundi tofauti kwa ajili ya michuano hiyo inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kuanza kwa mashindano ya CECAFA Kagame Cup ya mwaka 2025 – mashindano yanayowakutanisha vilabu kutoka Afrika Mashariki na Kati – timu ya jeshi la Rwanda, APR FC, imepangwa kwenye Kundi B.
Droo ya upangaji wa makundi ilifanyika Alhamisi hii, ambapo jumla ya timu 12 zitakazoshiriki ziligawanywa katika makundi matatu.
Kundi B linaundwa na APR FC (Rwanda), NEC FC (Uganda), Bumamuru FC (Burundi), na Mlandege FC kutoka Zanzibar.

Kundi A linajumuisha Harde Cote FC (Djibouti), Coffee SC (Ethiopia), Singida Big Stars (Tanzania), na Kenya Police FC (Kenya). Kundi C linaundwa na Al-Hilal (Sudan), Kator FC (Sudan Kusini)
Mogadishu City Club (Somalia), na Al-Ahly SC Wad Madani (Sudan).
Mashindano haya yanatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania kuanzia Septemba 2 hadi 15, 2025. Mechi zitapigwa katika viwanja mbalimbali vikiwemo Azam Complex, Chamazi, Isamuyo Stadium na uwanja wa KMC.

Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA, Auka Gecheo, amesema kuwa mashindano haya yatasaidia vilabu vya ukanda huu kujiandaa vyema kwa michuano ya kimataifa ya CAF Champions League na CAF Confederation Cup.
“Mashindano haya yatakuwa jukwaa la maandalizi kwa vilabu vyetu kabla ya kuanza kwa michuano ya CAF 2025/2026 itakayoanza mwakani,” alisema Gecheo.
CECAFA Kagame Cup lilichezwa mwaka jana ambapo Red Arrows kutoka Zambia waliibuka mabingwa baada ya kuifunga APR FC ya Rwanda kwenye mchezo wa fainali.
Bagabo John
