Waziri wa Afya, Dkt. Sabin Nsanzimana, amesema kuwa wasichana wanaopata ujauzito katika umri mdogo hukumbana na changamoto kubwa za kiafya kwa sababu miili yao huwa haijakomaa vya kutosha kwa ajili ya kujifungua. Hali hiyo husababisha wengi wao kuwa katika hatari kubwa ya kupoteza maisha wakati wa kujifungua.
Dkt Nsanzimana ameyataja hayo hii Leo Tarehe 26 Juni 2026 Katika Kongamano la ‘Jukwaa la Vijana’ lilofanyika katika Kigali Convention Centre, likiwakutanisha vijana kutoka sehemu mbalimbali za nchi kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya jamii.

Dkt. Nsanzimana alieleza pia kuwa watoto wanaozaliwa na wasichana hao wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kuzaliwa kabla ya wakati unaotakiwa, jambo linalowaweka kwenye mazingira magumu ya kiafya tangu wanapozaliwa.
Aidha, alisema kuwa watoto hao ndio wanaoongoza kwa kuwa na tatizo la udumavu, akisisitiza kuwa takribani theluthi moja yao hukumbwa na hali hiyo.

Alisema, "Theluthi moja ya watoto hawa hupata udumavu, na theluthi moja ya watoto wanaofariki kabla ya kutimiza muda wa kuzaliwa hutokana na mimba za utotoni.
Tatizo hili huendelea kuathiri familia na hatimaye taifa kwa ujumla."
Waziri huyo alisisitiza kuwa mimba za utotoni si tatizo linaloishia kwa mama na mtoto pekee, bali lina athari za muda mrefu kwa familia na maendeleo ya nchi, hivyo akatoa wito kwa jamii kushirikiana katika kuzuia mimba za utotoni na kulinda afya ya wasichana.
Bagabo John
