Wafungwa zaidi ya 5,000 walioko katika Gereza la Rwamagana wanatarajiwa kunufaika na huduma maalum za matibabu ya macho, hatua inayolenga kuboresha afya na ustawi wao wakiwa kifungoni.
Inatarajiwa kuwa zoezi hili litadumu kwa muda wa siku 10, ambapo zaidi ya wafungwa 5,000 watapokea huduma mbalimbali za afya.
Miongoni mwa huduma zitakazotolewa ni pamoja na upimaji wa macho na utoaji wa miwani maalum ya kusomea na kuona kwa wale watakaobainika kuwa na matatizo ya macho.
Aidha, wale watakaogundulika kuwa na matatizo makubwa ya kiafya watarejeshwa katika hospitali za rufaa kwa matibabu zaidi, bila kutozwa gharama yoyote.

Senior Superintendent Hillary Sengabo, ambaye ni msemaji wa Idara ya Magereza ya Rwanda (RCS), amesema kuwa zoezi hili linaandaliwa kwa namna ya kipekee, kwani madaktari huletwa moja kwa moja magerezani kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa wafungwa.
Ameeleza kuwa hii ni njia bora ya kuwafikia wafungwa wengi katika mazingira salama, tofauti na kuwasafirisha hadi hospitali ambako hukutana na umati wa watu.

"Hili si tukio la kwanza kufanyika, wala si la mwisho," alisema Sengabo. "Tumekuwa tukilifanya pia katika magereza mengine na kwa magonjwa mbalimbali, siyo macho tu. Zoezi hili litaendelea kama sehemu ya huduma zetu za afya kwa wafungwa."
Chanzo RCS
